Mjadala kuhusu athari za barabara ya reli ya kisasa SGR umezidi kupamba moto huku Mwakilishi wa kike wa Kaunti ya Kwale Bi Zuleikha Juma akishinikiza kusitishwa kwa ubaguzi wa kiuchumi uliyochangiwa na mradi huo.
Bi Juma amesema japo hakuna kiongozi wa Pwani anayeupinga mradi huo, ni vyema iwapo kutakuwepo na usawa katika ugavi wa biashara na shughuli za uchukuzi kati ya barabara hiyo ya reli ya kisasa na ile ya lami.
Kulingana na kiongozi huyo, sekta ya uchukuzi wa makasha kupitia barabara ya lami imesambaratika pakubwa huku mamia ya wakaazi wa Ukanda wa Pwani na Wakenya wengine wakipoteza ajira kutokana na hali hiyo.
Bi Juma amekariri kwamba athari hizo zitakuwa mbaya zaidi endapo serikali kuu haitarudi nyuma na kuifufua sekta hiyo ya uchukuzi wa malori ya masafa marefu akihoji kwamba jamii ya Pwani imetegemea mno sekta hiyo kiuchumi.
Kauli ya Zuleikha inajiri baada ya ripoti ya utafiti iliyozinduliwa hapo jana kubaini kwamba Kaunti ya Mombasa imesambaratika kiuchumi kufuatia mradi huo wa barabara ya reli ya kisasa SGR.