Zoezi la kuwapima Madereva wa masafa marefu virusi vya Corona mjini Voi na katika mpaka wa Kenya na Tanzania katika eneo la Taveta, litaanza rasmi baada ya kukamilika kwa mipangilio ya kulitekeleza zoezi hilo.
Gavana wa kaunti ya Taita Taveta Granton Samboja amelitaja zoezi hilo kama mwafaka katika jitihada za kukabiliana na virusi vya Corona katika kaunti hiyo.
Kulingana na Samboja, eneo la Voi limetumika na wahudumu wa magari ya masafa marefu, akionya kuwa iwapo Madereva hao hawatapimwa virusi hivyo basi wataiweka kaunti hiyo katika hatari.
Samboja amewataka wahudumu hao wa malori ya masafa marefu kutoghairi zoezi hilo, akisema sio tu kuwa lina umuhimu wa kuwalinda wakaazi wa kaunti ya Taita Taveta bali pia Madereva hao sawia na familia zao.