Story by Mwahoka Mtsumi –
Katibu mkuu msimamizi katika Wizara ya Afya nchini Dkt Mercy Mwangangi amezindua rasmi zoezi la utoaji wa chanjo ya ukambi kwa watoto wa kati ya umri wa miezi 9 hadi miaka 5.
Dkt Mwangangi amesema zoezi hilo linalenga watoto takriban milioni 3.5 huku akisema chanjo hiyo inatolewa bila malipo ili kuwapa kinga ya mwili watoto.
Akizungumza na Wanahabari baada ya uzinduzi huo katika kaunti ya Kajiado, Dkt Mwangangi amesema zaidi ya wahudumu wa afya 1,600 watazuru mashinani kutoa chanjo hiyo kwa watoto.
Amesema maeneo ya makanisa, misikitini, shuleni, maeneo ya umma na hata katika vituo vya afya ya umma ni kati ya vituo vilivyopendekezwa kutoa chanjo hiyo kwani zoezi hilo litatekelezwa katika kaunti 22 nchini, huku kaunti ya Kilifi na Tana river zikijumuishwa katika mpango huo.
Wakati huo huo amewahimiza wazazi walio na watoto wa chini ya umri wa miaka mitano kutopuuza zoezi hilo na badala yake kuwaruhusu watoto wao kupokea chanjo hiyo.