Picha kwa Hisani –
Chama cha ODM kimeandaa kura ya mchujo eneo bunge la Msambweni kaunti ya Kwale, ili kupata kiongozi atakaepeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mdogo wa kiti cha ubunge eneo hilo.
Zoezi hilo ambalo limeanza saa mbili asubui litakamilika mwendo wa saa kumi na moja jioni ya leo na wagombea wawili akiwemo Nicholus Zani na Omar Boga wanawania tiketi hio ya ODM.
Akizungumza baada ya kupiga kura katika kituo cha uwanja wa Jogoo Omar Boga ambae ni mmoja wa wagombea hao amelaumu wasimamizi wa zoezi hilo kwa kuchelewa kuwasilisha vifaa vya kupigia kura.
Kwa upande wake Nicholus Zani mmoja wa wagombea hao aliyezungumza baada ya kupiga kura katika kituo cha Mwakigwena ameeleza kuridhishwa kwake na jinsi zoezi hilo linavyoendeshwa.
Nao wapiga kura waliojitokeza kushiriki zoezi hilo wakiongozwa na ziporah Nyawera wamelalamika kwamba baadhi ya majina ya wapiga kura hayakujumuishwa kwenye sajili rasmi.
Hata hivyo katibu wa ODM eneo hilo Shabani Luchesi amekiri kukosekana kwa majina ya baadhi ya wapiga kura,akisema hatua hio imechangiwa na hatua ya maafisa rejeshi kutumia sajili ya ODM badala ya ile ya IEBC.
Uchaguzi huo mdogo wa kiti cha ubunge eneo la Msambweni utaandaliwa tarehe 15 ya mwezi Disemba na umewavutia wagombea kadhaa akiwemo Shehe Mahmoud Abdulrahman wa WIPER,Nicholus Zani,Omar Boga na Sharlet Akinyi Mariam na Feisal Dori.