Story by Mimuh Mohamed:
Serikali imetangaza kwamba zoezi la kufukua miili katika msitu wa Shakahola kaunti ya Kilifi litaendelea kuanzia mwezi wa Machi.
Kulingana na mpasuaji mkuu wa serikali Johansen Oduor, hii itakua awamu ya tano na ya mwisho ya kufukua miili ya watu hao wanaoaminika kuwa waumini wa mchungaji tata wa kanisa la Good News International Paul Mackenzie.
Oduor aidha amesema kufikia sasa wamefanyia upasuaji jumla ya miili 429 iliyofukuliwa katika msitu huo wa Shakahola, na wanasubiri matokeo ya uchunguzi wa vinasaba yaani DNA uliofanyiwa miili hiyo.
Oduor amesema matokeo ya uchunguzi wa DNA yatakuwa tayari kufikia mwezi ujao na wataikabidhi kwa familia miili yote itakayoweza kutambuliwa.
Kauli yake imejiri wakati ambapo mchungaji Paul Mackenzie na washukiwa wenza 94, wakiwa kizuizini wakikabiliwa na mashtaka mbali mbali ikiwemo mauaji, ugaidi, unyanyasaji wa haki za watoto miongoni mwa mashtaka mengine.