Mgogoro katika ya Watetezi wa haki za kibinadamu na bunge la Kaunti ya Mombasa sasa umemfikia afisa mkuu mtendaji wa tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini, Twalib Mbarak aliyetakiwa kuchunguza kwa kina ziara ya wajumbe 9 wa bunge hilo hadi nchini Misri kutazama kipute cha mabingwa wa soka Barani Africa AFCON.
Katika barua rasmi iliyoandikwa kwa tume ya EACC, Watetezi hao wanamtaka Mbarak kuanzisha uchunguzi huo mara moja kufuatia madai ya ufujaji wa fedha za umma unaotekelezwa na Viongozi hao.
Mashirika hayo likiwemo lile la Haki Afrika, Huria, Manyatta Youth Entertainment na Pwani Social Justice Centres Working Group yamesema kwamba safari ya wajumbe hao kamwe haikuwa na msingi wowote wala hakuna lolote muhimu walilokwenda kusoma ziarani humo na badala yake wamekuwa wakipiga picha na wacheza densi wakijifurahisha.
Mkurugenzi mkuu wa Haki Afrika Hussein Khalid amedokeza kwamba safari hiyo imemgharimu mlipa ushuru kima cha shilingi milioni 3.2 kwa Wawakilishi wadi hao kuzuru Misiri bila ya fedha hizo kujumuishwa katika bajeti ya kima cha shilingi bilioni 13.4 kilichopitishwa kisiri hivi majuzi na bunge hilo licha ya kupingwa na Wakaazi.
Khalid amesema kwamba kamwe Mashirika hayo ya utetezi wa haki hayatawalegezea kamba wajumbe hao bali italifuatilia kikamilifu swala hilo.