Story by Janet/Gabriel –
Zaidi ya familia 200 katika kijiji cha Mwamdudu eneo bunge la Kinango kaunti ya Kwale zimeachwa bila makao baada ya nyumba zao kubomolewa chini ya ulinzi mkali wa maafisa wa polisi.
Familia hizo zikiongozwa na Clinton Munga, zimesema maafisa wa polisi wameingia katika kijiji hicho usiku wa manane na kuongoza shughuli ya uzibomozi wa nyumba zao, zoezi wanalosema limetekelezwa pasi na kupewa notisi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa wakaazi hao Hamis Mwero, amesema shule ya pili ya Mwamdudu na Kanisa ni miongoni mwa nyumba zilizobomolewa na kuwaacha wenyeji bila makao.
Mwero ameweka wazi kwamba wakaazi wataandamana na kutatiza shughuli zote za uchukuzi katika barabara kuu ya Mombasa -Nairobi kila siku hadi pale watakapofahamishwa aliyenyakua ardhi yao.
Hata hivyo Afisa mkuu wa polisi eneo la Kinango Fredrick Ombaka amethibitisha kwamba polisi wameongoza ubomozi huo akisema wamepewa kibali cha Mahakama kuwaondoa wakaazi katika ardhi hiyo yenye ekari takriban 500.