Picha Kwa Hisani.
Mkongwe wa sanaa ya muziki Z Anto ambaye aliwahi kutamba na ngoma ya Binti Kiziwi, amefichua sababu zake za kukaa kimya kwa muda mrefu na kueleza kuwa alikuwa anaandaa nyimbo za kumrejesha kwa kishindo.
Ameeleza kuwa amekuwa akiandaa albamu mpya yenye nyimbo sita, anayotarajia kuachia wakati wowote kuanzia sasa.
Msanii huyo aliweka wazi kuwa video za ngoma hizo sita ziko tayari ingawa majadiliano kuhusu jina la albamu na wasimamizi wake bado yanaendelea.
“Nilikuwa chimbo kuandaa mawe, zitakuwa kazi nzuri maana nimefanya na wasanii tofauti ambao watakuwa sapraizi siku ambayo nitaachia kazi zangu, ambazo nitaziuza sana online kuliko kwa mfumo wa albamu ambao kibiashara ni ngumu kwasasa, kutokana na sayansi na tekinolojia inavyokuwa kwa kasi” Alieleza Z Anto
Ameongeza kuwa “Muziki unahitaji ubunifu na kuyasoma mazingira kwa wakati tuliopo,ndio maana nilipata muda wa kujua nahitaji kuipa ujumbe gani jamii, kisha nikaanza kuyafanyia kazi yale niliyoyaona kwamba yanafaa kwa wakati gani.”
Mbali na hilo, amegusia changamoto iliopo kwenye sanaa kwamba bila kuandika ujumbe wa kueleweka, unakosa mapokezi mazuri kutoka kwa mashabiki.
“Muziki ni maisha ndio maana kuna wakati ambapo mtu anapenda mdundo ili kupata mzuka wa kucheza, kuna wakati wa kusikiliza ujumbe ili umfunze na kumfariji, hivyo vyote lazima msanii avizingatie na kwa wakati sahihi,”alieleza Z Anto.