Wizara ya Elimu katika kaunti ya Kwale imesema inaendeleza mikakati ya kuhakikisha shule za chekechea zinajengwa katika maeneo yote ya mashinani yanayoshuhudia uhaba wa shule hizo.
Waziri wa elimu katika serikali ya kaunti ya Kwale Mangale Chiforomodo amesema hatua hiyo itasaidia kuwawezesha watoto kujiunga na shule hizo wakiwa na umri mdogo.
Chiforomodo amesema hatua hiyo inalenga kupunguza pia idadi kubwa ya wanafunzi wanaokamilisha masomo ya darasa la nane wakiwa na umri mkubwa zaidi.
Wakati uo huo amesisitiza kwamba viwango vya elimu katika kaunti ya Kwale vinazidi kuimarika kwani jamii ya kaunti hiyo imetambua umuhimu wa masomo.