Picha kwa Hisani –
Wizara ya Afya nchini imesema inashirikiana na taasisi mbalimbali za utafiti wa kimaabara kutoka humu nchini na zile za kimataifa ili kuibuka na chanjo ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona.
Katibu mkuu msimamizi katika Wizara hiyo Dkt Mercy Mwangangi, amesema Kenya inashiriki katika majaribio ya tafiti mbalimbali ili kuhakikisha chanjo inayozinduliwa na wataalam wa kiafya ni salama kwa wakenya.
Akigusia takwimu za maambukizi ya virusi vya Corona, Dkt Mwangangi amesema watu 379 wamethibitishwa kupata virusi hivyo baada ya sampuli 3,867 kufanyiwa uchunguzi na idadi hiyo kuongezeka hadi watu 31,015.
Dkt Mwangangi amesema kati ya watu hao 379, watu 372 ni wakenya huku watu 7 wakiwa raia wa kigeni na wanaume ni 223 huku wanawake wakiwa 156 na mtoto wa mwako mmoja ni kati ya walioambukizwa virusi hivyo ndani ya saa 24.
Katibu huyo amedokeza kuwa watu 244 waliokuwa wakiugua ugonjwa huo wamepona na kupelekea idadi hiyo kufikia watu 17, 612 huku watu 19 wakiaga dunia.