Wizara ya Afya nchini imeweka wazi kwamba kufikia sasa wahudumu wa afya 4,698 wamepata maambukizi ya virusi vya Corona huku 2,562 kati yao wakiwa ni wanawake na wanaume wakiwa 2,136.
Katika taarifa iliotumwa kwa vyombo vya habari, Wizara hiyo imesema tangu janga la Corona liripotiwe humu nchini wahudumu wa afya 38 wameaga dunia.
Wizara hiyo imedokeza kuwa watu 629 wamethibitishwa kupata maambukizi hayo hii leo, baada ya sampuli 5,832 kufanyiwa uchunguzi na kuchangia idadi hiyo kufikia watu 152,523.
Hata hivyo watu 1,560 wamethibitishwa kupona virusi vya Corona na idadi hiyo kufikia watu 103,838 huku watu 18 wakitangazwa kuaga dunia.
Wakati uo huo Wizara hiyo imetangaza kwamba watu 721,509 tayari wamepokea chanjo ya kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona huku watu 407,711 wakiwa wa umri wa miaka 58 na zaidi.