Wizara ya afya nchini imezifunga jumla ya hospitali 10 za kibinafsi katika Kaunti ya Kilifi kutokana na kutotimiza masharti ya wizara hiyo.
Naibu Mkurugenzi wa huduma za kimatibabu katika wizara hiyo Dkt Jackson Kioko amesema kwamba hospitali hizo zimeyaweka maisha ya wagonjwa hatarini.
Kioko amesema jumla ya maduka 11 ya kuuza dawa pia yamefungwa mjini Mtwapa kwa kuendeleza shughuli zao bila vibali hitajika kutoka kwa bodi ya dawa na sumu nchini.
Daktari Kioko amehoji kwamba oparesheni hiyo imeimarishwa kutokana na ulaghai unaoendelezwa na watu wanaojifanya kuwa wahudumu wa afya japo hawahitimu.
Amedokeza kwamba wamezifunga hospitali tano za kibinafsi katika Kaunti ya Mombasa na maduka kadhaa ya kuuza dawa katika oparesheni hiyo itakayoendelezwa kwa kipindi cha miezi mitatu kote nchini.
Taarifa na Gabriel Mwaganjoni.