Picha kwa Hisani –
Huku maadhimisho ya wiki ya kimataifa ya kunyonyesha mtoto yakiendelea shirika la afya duniani WHO limesema lazima akina mama wapewe motisha ili wakumbatie unyonyeshaji wa watoto wao wachanga kwa miezi sita mfululizo.
Mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros Adhanom amesema licha ya kunyonyesha kuwa na faida za kiafya kwa mama na mtoto ni asilimi 40 pekee ya watoto wa miezi 0 hadi 6 wanaonyonyeshwa ulimwenguni.
Tedros amesema kina mama wanafaa kuelimishwa umuhimu wa kunyonyesha watoto wao akisema maisha ya watoto zaidi ya laki 8 elfu 20 walio na umri wa chini ya miaka 5 yanaweza kunusurika kila mwaka,iwapo watanyonyeshwa ipasavyo.
Nalo shirika watoto la umoja wa mataifa UNICEF kupitia mkurugenzi wake Harriet Fore limesema ukosefu wa sera za kuunga mkono unyonyeshaji ikiwemo likizo yenye malipo kwa wazazi kumerudisha nyuma uwezo wa akina mama kunyonyesha watoto kwa muda hitajika.
Ripoti ya UNICEF ya mwaka 2019 imeeleza kwamba unyonyeshaji una faida kubwa kwa mama na mtoto ikiwemo uimarishaji wa afya ya akili katika maendeleo ya mtoto, kuwalinda watoto dhidi ya magonjwa, na pia kuwalinda akina mama wanaonyonyesha dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi na ya matiti.