Story by Mimuh Mohamed
Shirika la afya duniani WHO limehimiza uwekezaji na uvumbuzi wa vifaa na dawa zitakazoongeza kasi ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria.
Katika taarifa kwa Wanahabari mkurugenzi wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesu amesema ugonjwa wa malaria ambao unazuilika na kutibika umeleta madhara mengi kwa afya na maisha ya watu wengi ulimwenguni.
Kulingana na ripoti ya WHO ya mwaka 2020, jumla ya visa vipya milioni 241 vya maambukizi ya malaria na vifo elfu 627 vinavyotokana na ugonjwa huo vilinakiliwa.
Ghebreyesus amesema zaidi ya tuluthi mbili wa vifo hivyo vilihusisha watoto wenye umri wa chini wa miaka mitano wanaoishi barani Afrika.
WHO imesema licha ya vita vya kumaliza maambukizi kati ya mwaka 2002 na 2015, katika miaka ya hivi karibu mapambano hayo yamedorora na kwamba juhudi zinahitaji kuwekezwa kutimiza ruwaza ya mwaka 2030 ya mkakati wa malaria wa WHO.
Haya yanajiri wakati ulimwengu unaadhimisha siku ya malaria duniani halfa ambayo huandaliwa tarehe 25 mwezi Aprili kila mwaka.