Ni sharti walanguzi wa dawa za kulevya waandamwe na watiwe nguvuni kwa kuwa wamesambaratisha maisha ya vijana wengi katika Kaunti ya Mombasa.
Waziri wa maswala ya Vijana, Jinsia na Michezo wa Serikali ya Kaunti ya Mombasa, Munywoki Kyalo amesema kwamba hali ya vijana katika Kaunti ya Mombasa ni ya kusikitisha kwani vijana wengi wamezama katika uraibu wa dawa za kulevya na kushiriki uhalifu.
Akiwahutubia vijana katika ukumbi wa Tononoka Mjini humo wakati wa maadhimisho ya siku ya Vijana ulimwenguni, Kyalo ameshikilia nabila ya juhudi kuimarishwa kwa lengo la kuikabili hali hiyo basi kizazi kichanga kitaangamizwa na Kaunti ya Mombasa kusalia katika hali ya chini kimaendeleo.
Hata hivyo, Kyalo anasema kwamba serikali ya Kaunti hiyo inawekeza katika matibabu kwa waraibu wa dawa za kulevya ili kuwanasua kutoka kwa hali hiyo na kuwafanya watu muhimu wa kutegemewa na jamii.