Story by Bakari Ali –
Waziri wa Elimu nchini Prof George Magoha amesisitiza kuendelezwa kwa mfumo mpya wa elimu wa CBC, akisema mfumo huo ni miongoni mwa mifumo bora zaidi ya elimu kote duniani.
Akizungumza katika halfa ya kuwatunuku wanafunzi walioshiriki mashindano ya uandishi yalioandaliwa na Kampuni ya Pwani Oil, Waziri Magoha amesema Wizara ya elimu nchini haina mipango ya kuusitisha mfumo huo.
Waziri Magoha amesema Wizara ya elimu nchini iko tayari kushirikiana na wadau wa sekta ya elimu kuutetea mfumo huo Mahakamani, akihoji kwamba tayari walimu wameukumbatia mfumo huo kutokana na mafunzo waliopokea.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maswala ya biashara katika kampuni hiyo Rajul Malde ameunga mkono kauli ya Magoha, akisema kuna haja ya wadau wa sekta ya elimu kushirikiana na kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora.
Hata hivyo Waziri wa Utalii nchini Najib Balala aliyehudhuria halfa hiyo amesisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya serikali, wawekezaji na wadau mbalimbali ili kusazidia jamii zisizo na uwezo katika maswala ya elimu.