Picha kwa hisani –
Waziri wa Elimu nchini Profesa George Magoha amepuuzilia mbalimbali taarifa iliotolewa na taasisi ya utafiti wa kimatibabu nchini KEMRI kwamba maambukizi ya virusi vya Corona shuleni yataongezeka ifikapo mwezi Machi.
Waziri Magoha amesema taarifa hizo hazina msingi wowote na zinalenga kuwatia hofu wazazi, huku akiwahakikisha wazazi kuwa usalama wa wanafunzi dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona umeangazia kikamilifu.
Katika kikao na Wanahabari kule Mombasa, Waziri Magoha amesema katika ziara alizozifanya katika shule mbalimbali nchini, amebaini kuwa wanafunzi wako salama na wanazingatia masharti yote ya kiafya yaliowekwa ikiwemo kuvaa barakoa, kuonyesha mikono sawia na umbali wa mita moja shuleni.
Waziri Magoha amewahakikishia wakenya kwamba juhuzi zinazoendelezwa na serikali za kutokomeza virusi vya Corona nchini zitafaulu huku akihimiza kila moja kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi hivyo.
Mapema hapo jana, Taasisi ya utafiti wa kimatibabu nchini KEMRI kupitia Afisa mkuu wa taasisi hiyo Daktari Charles Agoti, ilisema kufikia mwezi Juni mwaka huu visa vya maambukizi ya Corona vitaongezeka shuleni kwa asilimia 25.