Story by Our Correspondents-
Waziri wa Afya nchini Mutahi Kagwe amesema serikali imeafikia hatua ya kuwatuma wahudumu wa afya wa ziada katika mataifa ya nje baada ya serikali kupitia Wizara hiyo kubaini kwamba Kenya ina wahudumu wa afya wa kutosha.
Akizungumza baada ya kuzindua mafunzo ya lugha ya Kiingereza kwa wahudumu wa afya katika taasisi ya KMTC jijini Nairobi, Waziri Kagwe amesema kila mwaka zaidi ya wauguzi elfu nne hufuzu katika taaluma hiyo na kuchangia Kenya kuwa na wahudumu wa afya wa kutosha.
Kagwe amedokeza kwamba kuzinduliwa kwa mafunzo hayo kwa wahudumu wa afya kutasaidia wauguzi kupata nafasi za ajira katika mataifa ya Ulaya kwani mwaka uliopita ni wauguzi 10 pekee kati ya 300 waliopita mtihani wa Kiigereza na kwenda kufanya kazi nchini Uingereza.
Wakati uo huo Wizara ya Afya nchini imedokeza kwamba watu 171 wamethibitishwa kupata maambukizi ya virusi vya Corona baada ya sampuli 6,137 kufanyiwa uchunguzi na idadi hiyo kufikia watu 321,552.
Hata hivyo wagonjwa wa Corona 137 wamethibitishwa kupona na kuchangia idadi hiyo kufikia watu 294,859 huku wale walioaga dunia kutoka na makali ya Corona ikifikia watu 5,587.