Picha kwa hisani –
Waziri wa Afya nchini Mutahi Kagwe, amesema Wizara ya Afya pamoja na wadau wengine wa maswala ya kiafya humu nchini wako mbioni kuhakikisha chanjo ya kudhibiti virusi vya Corona inawasili nchini.
Akizungumza na Wanahabari baada ya kutia saini mkataba wa Makubaliano na maafisa wa kliniki ambao wamesitisha rasmi mgomo wao, Waziri Kagwe amesema chanjo hiyo itawasili nchini mwezi Februari mwaka huu wa 2021.
Waziri Kagwe imezidi kuwaonya wakenya dhidi ya tabia ya kupuuza masharti ya kujikinga na virusi vya Corona, akisema mwezi huu wa Januari idadi ya maambukizi inatarajiwa kuongezeka kutokana na sherehe za mwisho wa mwaka zilizoshuhudia mikusanyiko ya watu.
Akigusia takwimu za maambukizi ya virusi vya Corona, Waziri Kagwe amesema watu 156 wamethibitishwa kupata maambukizi hayo kutokana na sampuli 4,317 na idadi hiyo kufikia watu 96,614.
Hata hivyo amedokeza kuwa watu 65 waliokuwa wakiugua virusi hivyo wamethibitishwa kupona na idadi hiyo kufikia watu 78,802 huku watu 11 wakitangazwa kuaga dunia.