Picha kwa Hisani –
Waziri wa Afya nchini Mutahi Kagwe amevitaka vyombo vya habari nchini kuhakikisha vinawatafuta wataalum wa maswala ya kiafya wakati wanapotaka ufafanuzi zaidi kuhusu magonjwa mbalimbali hasa wakati huu wa janga la Corona.
Akizungumza katika makao makuu ya Muungano wa Madaktari nchini KMPDU, Waziri Kagwe amesema sio madaktari wote walio na ufahamu wa magonjwa yote ulimwenguni bali kila daktari ana taalum aliyobobea nayo.
Wakati uo huo amezidi kuwaonya wakenya wanaopenda kuzuru katika vilabu vya pombe, baa na mihakawa kutumia vileo, akiwataka kujitenga na sehemu hizo na badala yake kutumia fedha za kununua pombe kusaidia familia zao.
Akigusia takwimu za maambukizi ya Corona, Waziri Kagwe amesema Kenya imenakili visa 19,125 vya maambukizi ya Corona baada ya watu 544 kuthibitishwa kupata maambukizi hayo kutokana na sampuli 5,259 zilizofanyiwa uchunguzi.
Wakati uo huo amesema watu 113 wamethibitishwa kupona virusi hivyo na idadi hiyo kufikia watu 8,021 huku watu 12 wakiaga dunia.