Waziri wa Afya nchini Mutahi Kagwe amefanya ziara ya kiafya katika hospitali za kaunti ya Taita Taveta kukagua mikakati ilioidhinishwa na serikali ya kaunti hiyo kudhibiti msambao wa virusi vya Corona.
Waziri Kagwe amesema zoezi la kuwachanja wakenya chanjo ya kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona linaendelea vyema japo idadi ya wakenya wanaojitokeza kupokea chanjo hiyo imeanza kushuka.
Akizungumza katika eneo la Mwatate kaunti ya Taita taveta, Waziri Kagwe amesema kufikia sasa Kenya imewachanja watu 853,081 huku watu wa umri wa miaka 58 na zaidi wakiandikisha idadi ya watu 494,278.
Hata hivyo amesema juhudi zinazoendelezwa na serikali ya kaunti ya Taita taveta za kupambana na maambukizi ya Corona ni za kuridhisha huku akiwahimiza wakenya kutopuuza masharti ya kujikinga na Corona.
Wakati uo huo Wizara ya Afya nchini imethibitisha kwamba watu 834 wamepata maambukizi ya virusi vya Corona katika mda wa saa 24 baada ya sampuli 8,498 kufanyiwa uchunguzi na idadi hiyo kufikia watu 158,326 huku watu 579 wakithibitishwa kupona virusi hivyo na watu 23 wakiaga dunia.