Taarifa na Charo
Waziri wa afya kaunti ya Kilifi Daktar Anisa Omar pamoja na maafisa wakuu wa wizara hio wamejipata pabaya baada ya kushindwa kueleza mbele ya kamati ya bunge la kaunti hio kuhusu afya ,kiini cha kufariki kwa mtoto wa siku nne katika hospitali ya kaunti ndogo ya Malindi wiki moja iliopita.
Akiongea mbele ya Kamati hiyo iliyokuwa ikiongozwa na spika wa bunge la kaunti ya Kilifi Jimmy Kahindi Bi Anisa amekiri kuwa baaadhi ya wauguzi na madaktari katika hospitali za Malindi na Kilifi wanamatatizo ya kiakili hali inayopelekea wakaazi kupata huduma duni za afya.
Viongozi wa kaunti hio wakiongozwa na mwakilishi wa wadi ya Kakuyuni Nixon Mramba wamesema ni lazima wahudumu wa afya ambao hawana uwezo wa kuwahudumia wakazi watimuliwe mara moja.
Hata hivyo spika wa bunge la Kilifi Jimmy Kahindi ameipa idara ya afya ya kaunti hio majuma matatu kuwasilisha ripoti kamili kuhusu madai ya kukosekana kwa hewa ya Oxygen kwenye hospitali hiyo hatua inayodaiwa kusababisha kifo cha mtoto huyo juma moja lililopita.