Onyo kali limetolewa kwa wazazi wanaowaficha watoto wao licha ya kufahamu bayana kwamba wanashiriki uhalifu kwamba watakabiliwa kikamilifu.
Kamanda mkuu wa polisi wa Kaunti ya Mombasa Augustine Nthumbi amesema mara nyingi msimu huu wa Likizo vijana wadogo hasa wa eneo la Kisauni hushiriki uhalifu huku wazazi wao wakisalia kimya licha ya kufahamu bayana kwamba wanao wamejiunga na magenge ya kihalifu.
Akizungumza Mjini Mombasa hii leo, Nthumbi amesema hali hiyo kamwe haitavumiliwa na kikosi maalum cha Maafisa wa usalama kimetumwa hasa katika eneo la Kisauni ili kuyakabili magenge hayo ambayo katika siku za hivi majuzi yamechangia msukosuko wa kiusalama katika Gatuzi hilo dogo.
Nthumbi amewataka Wazazi wa eneo hilo la Kisauni kujitayarisha kwa wakati mgumu mno kwani watoto wao watakaoshiriki uhalifu kamwe hawatasazwa bali kusambaratishwa akihoji kwamba oparesheni iliyoanza hapo jana baada ya lalama kutoka kwa Wanafunzi wa chuo kikuu cha TUM kamwe haitasitishwa hadi Vijana hao wakabiliwe.
Wakati uo huo, amehoji kwamba Maafisa wa usalama wanaliandama genge la Vijana kumi ambalo limekuwa likijihami kwa visu na mapanga na kuwajeruhi Wakaazi na hasa Wanafunzi wa chuo kikuu cha TUM wanaoishi katika eneo hilo la Kisauni.