Onyo kali limetolewa kwa wazazi wa Wadi ya Ziwa la Ng’ombe, Nyali kaunti ya Mombasa kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria endapo watoto wao watapitia dhulma za kimapenzi msimu huu wa likizo.
Mwanaharakati wa maswala ya jinsia na haki za watoto katika eneo bunge hilo Miriam Kimemia amesema eneo hilo limekuwa likirekodi visa vingi vya watoto kudhulumiwa kingono bila ya wazazi kujali, akisema wazazi hao wataadhibiwa.
Akizungumza na Wanahabari, Miriam amewatahadharisha wazazi dhidi ya kuzembea katika kuyatekeleza majukumu yao, akiwataka wawachunge watoto wao vyema.
Mwanaharakati huyo hata hivyo amewasihi watoto kuondoa hofu na kuwashtaki Wazazi wao au walezi wanaowadhulumu haki zao za kimsingi ili watu hao wachukuliwe hatua.
Taarifa na Gabriel Mwaganjoni.