Story by Gabriel Mwaganjoni-
Wavuvi watatu raia wa Tanzania wameokolewa katika maji makuu ya bahari hindi baada ya boti lao kusombwa na mawimbi makali.
Kulingana na taarifa kutoka kwa idara ya upelelezi nchini, watatu hao Hafidh Abdallah wa umri wa miaka 17, Musa Silima wa miaka 18 na Silimani Zidini walirauka alfajiri kwenda kuvua samaki baharini japo walipigwa na mawimbi makali kabla ya boti lao kupinduka.
Watatu hao wanaotoka katika kijiji cha Tanagani, Ksiwani Pemba katika mji mkuu wa Zanzibar walijizatiti na kuliwahi boti lao japo vifaa vyao vilikuwa vimesombwa na maji na wakasukumwa na mawimbi hadi maji makuu ya bahari hindi.
Watatu hao wamedai kwamba walizama maji tangu siku ya Jumamosi ndipo wakaokolewa na nahodha wa meli ya mizigo iliyokuwa ikielekea katika bandari ya Mombasa ya MV-Ince Atlantic na sasa wako katika hali nzuri ya kiafya baada ya kufanyiwa ukaguzi wa kiafya.
Tayari ubalozi wa Tanzania nchini Kenya umefahamishwa kuhusu tukio hilo na ukabaini kwamba watatu hao wanatokea kijiji cha Tanagani kisiwani Pemba na mipangilio ya kuwarudisha nyumbani imekamilika.