Shughuli za uvuvi katika Kaunti ya Lamu zimepigwa jeki hii leo baada ya Shirika la Msalaba mwekundu nchini kuwakimu wavuvi kwa vifaa vya thamani ya shilingi milioni 13.
Akizungumza huko Kizingitini wakati wa hafla ya kuwakabidhi wavuvi vifaa hivyo vikiwemo makatoni maalum ya kuhifadhia samaki, mashini maalum za kusukuma maboti, vyavu, miongoni mwa vifaa vinginevyo vya uvuvi, Naibu katibu mkuu wa Shirika hilo Dakta Asha Mohammed amesema vifaa hivyo vitawasaidia wavuvi hao kuendeleza shughuli zao.
Kulingana na Dakta Mohammed, mara nyingi wavuvi katika Kaunti hiyo hushindwa kutekeleza shughuli zao za uvuvi kutokana na ukosefu au kuwa na vifaa duni visivyoweza kuwafikisha kwenye maji makuu ili kupata mavuno mengine ya samaki.
Bi Mohammed amekariri kwamba ni sharti shughuli kama hivo ziungwe mkono hasa ikizingatiwa kwamba zimebuni ajira kwa mamia ya Wakaazi na hasa Vijana wa Kaunti hiyo ya Lamu.
Kwa upande wake, Naibu gavana wa Kaunti ya Lamu Abdulhakim Aboud amesema Serikali ya Kaunti ya Lamu itashirikiana na Shirika hilo la huduma za kibinadamu ili kuimarisha maisha ya jamii ya Kaunti hiyo ya Lamu hasa wavuvi.