Zaidi ya wavuvi elfu 3 eneo la Ngomeni kaunti ya Kilifi, wanaitaka idara ya uvuvi nchini kuingilia kati ili kuwaokoa kutokana na masaibu wanayopitia pindi wanapokuwa katika shughuli zao za uvuvi.
Wavuvi hao wakiongozwa na Kiongozi wao Shelali Mohamed, wamesema shughuli za uvuvi zimekumbwa na changamoto ikiwemo ukosefu wa maboti ya uokozi pindi wanapopatikana na dharura baharini.
Shelali amehoji kuwa hatua ya idara ya uvuvi nchini pamoja na viongozi kukosa kuwashughulikia wavuvi hao pindi wanapotoa lalama zao, imechangia pakubwa shughuli za uvuvi kusambaratika katika eneo hilo.
Shelali sasa anaitaka idara husika kuingilia kati swala hilo, akisema eneo la Ngomeni ndio eneo lenye kuvuliwa samaki wengi katika eneo zima la Pwani huku akidai kuwa kusambaratika kwa shughuli hizo huenda kukawaacha wakaazi wa eneo hilo bila ajira.
Taarifa na Charo Banda.