Story Gabriel Mwaganjoni –
Mwakilishi wa kike kaunti ya Lamu Ruweida Obo amewahakikishia wavuvi walioathirika na mradi wa LAPSET katika kaunti hiyo kwamba watafidiwa.
Ruweida amesema amewasilisha swala hilo katika Wizara ya uchukuzi nchini inayosimamia mradi huo wa LAPSET na ambao ndio chanzo cha wavuvi hao kutimuliwa kwenye maeneo yao ya uvuvi ili kutoa nafasi ya ujenzi wa mradi huo.
Akizungumza Kisiwani Amu, Ruweida ameikosoa Serikali kwa kuwabagua wavuvi katika swala la fidia, licha ya wao kuwachwa katika hali ya umaskini baada ya shughuli zao za uvuvi kusharibiwa na mradi huo wa bandari ya Lamu.
Ruweida amesema atafanya kila juhudi ili kuhakikisha wavuvi hao wamelipwa fidia kwani wavuvi hao wamekuwa wakidai fidia yao ya shilingi bilioni 1.7 yapata miaka 9 sasa baada ya wao kufurushwa kwenye maeneo yao ya uvuvi.