Story by: Gabriel Mwaganjoni
Waumini wa Kanisa katoliki kote ulimwenguni wamemiminika makanisa kuadhimisha ibada ya Misa ya Jumatano ya majivu.
Ibada hiyo inaashiria kuanza rasmi kwa kipindi cha Kwaresma ambapo Waumini hao hufunga kula na kunywa na kuzidisha ibada sawa na kutubia dhambi zao kwa kipindi cha siku 40 kabla ya maadhimisho ya Sikukuu ya Pasaka.
Askofu mkuu wa Kanisa katoliki jimbo kuu la Mombasa Martin Kivuva ameongoza ibada hiyo ya Misa katika kanisa katoliki la Holy Ghost Cathedral mjini Mombasa na amewapaka majivu waumini kwenye paji la uso.
Aidha amewasihi wakristu kuzidisha ibada zao, kufunga na kuomba na kujiweka karibu na wasiojiweza katika jamii sawa na kuliombea taifa ili wakenya wajitenge na malumbano na migawanyiko ya kisiasa.
Askofu Kivuvu ambaye pia ni Mwenyekiti wa kitaifa wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini amezidi kuwashambulia wanasiasa, akisema wamelirudisha taifa hili katika joto la kisiasa na mabishano ambayo ni dhahiri wazi kwamba yamewaganya wakenya katika misingi ya vyama vya kisiasa.
Hata hivyo Ibada sawa na hiyo imefanyika katika kanisa la kianglikana vile vile wito ukitolewa kwa waumini wa Kanisa hilo kuzidisha ibada, kutubia dhambi zao na kuliombea taifa wakati huu wa mfungo.