Story by Gabriel Mwaganjoni –
Maafisa wa polisi katika kaunti ya Kilifi wanawazuilia washukiwa watatu wa mauaji ya watu watatu.
Mshirikishi mkuu wa utawala Kanda ya Pwani John Elungata amesema watatu hao wanashukiwa kuhusika na mauaji ya Baba, Mwana na mfanyakazi wao waliokuwa wamezuru shambani mwao katika eneo la Junju huko Kilifi.
Hata hivyo, kulingana na Elungata wakaazi walidhani watatu hao walikuwa watekaji nyara na wakawapiga hata wakafariki na kisha kuliteketeza moto gari lao.
Elungata aliyekuwa akizungumza katika Kaunti ya Mombasa amewaonya vikali wakaazi wa eneo la Pwani dhidi ya kuchukua hatua mikononi mwao, akisema polisi wanaliandama vilivyo swala la utekaji nyara na halifai kuangaziwa visivyo na umma.
Kauli ya Elungata inajiri huku polisi wakimzuilia Joseph Wafula kijana wa umri wa miaka 23 anayedaiwa kuwahadaa mabinti katika eneo la Bamburi na kisha kuwateka nyara na kuwadhulumu kingono.