Story by Gabriel Mwaganjoni –
Watu watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Mombasa wakikabiliwa na mashtaka ya kukwepa kulipa ushuru wa kima cha shilingi milioni 34.5.
Inadaiwa kwamba watatu hao Habib Nkuliyingoma, Kennedy Komba na Esther Ngomo katika siku tofauti waliingiza makasha 23 ya bidhaa mbalimbali nchini ya thamani ya shilingi milioni 70.6 huku wakihadaa kwamba makasha hayo yalikuwa yanaelekezwa nchini Sudan Kusini.
Katika Shtaka la kwanza, Habib akiwa na mwenzake kwa jina la Danlystone Neil Kusumo ambaye hakuwa mahakamani, mnamo Disemba 20 mwaka wa 2017 na Machi 22 mwaka wa 2018 walikwepa kulipa ushuru wa shilingi milioni 11.3.
Katika shtaka la pili inadaiwa Habib, Komba na Ngomo kati ya mwezi Januari tarehe 7 na Januari 26 mwaka wa 2017 walikwepa kulipa ushuru wa kima cha shilingi milioni 5.3.
Na katika shtaka la tatu, kati ya mwezi Juni 29 na Novemba 21, Komba na Habib walikwepa kulipa ushuru wa kima cha shilingi milioni 17.8, ushuru wote katika mashtaka hayo matatu ukifikia kima cha shilingi milioni 34.5.
Kennedy na Habib wameachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni moja na mdhamini wa kiasi sawa na hicho kila mmoja huku Ngomo akiwachiliwa kwa dhamana ya shilingi elfu 50 na mdhamini wa kiasi sawa na hicho vile vile.
Kesi hizo tatu tofauti zitatajwa Juni 4, Juni 17 na terehe mosi mwezi Julai mwaka huu.