Story by Gabriel Mwaganjoni –
Watu watano wameaga dunia baada ya kuhusika katika ajali ya barabarani katika eneo la ‘Shangia Kwa Kajefa’ kwenye barabara kuu ya Mombasa -Nairobi.
Afisa mkuu wa polisi eneo la Rabai Ezekiel Chepkwony amesema dereva wa gari la kibinafsi lililokuwa likitoka Nairobi likielekea Mombasa huku lori likitoka Mombasa likielekea Nairobi yamegongana ana kwa ana na kusababisha maafa hayo.
Chepkwony amesema japo dereva wa gari dogo amejaribu kutoka barabarani ili kukwepa ajali hiyo, lori hilo tayari lilikuwa limefika na kuligonga gari hilo ambapo watu wawili wamefariki papo hapo na wengine watatu wakafariki katika hospitali ya Mariakani.
Watu wengine watano wamejeruhwa vibaya katika ajali hiyo na wanaendelea kupokea matibabu ya dharura katika hospitali ya Mariakani, kaunti ya Kilifi.
Magari yote mawili yameondolewa katika eneo la ajali na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Mariakani, huku miili ya watatu hao ikihifadhiwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali kuu ya Ukanda wa Pwani.