Jumla ya vijana 56 wameuwawa katika hali tatanishi mikononi mwa Maafisa wa usalama tangu mwanzoni mwa mwaka huu katika kaunti ya Mombasa pekee.
Mwenyekiti wa Shirika la utetezi wa haki za kibinadamu la MUHURI Khelef Khalifa ameitaja hali hiyo kama inayotia wasiwasi wakaazi wa kaunti ya Mombasa hasa baada ya tukio la usiku wa kuamkia leo ambapo vijana watatu waliuwawa kwa kupigwa risasi katika eneo la Utange kule Kisauni.
Khelef ameelezea hayo katika hospitali kuu ya Ukanda wa Pwani baada ya ripoti ya uchunguzi wa maiti kuonyesha kuwa Bilal Masoud Ndaro wa umri wa miaka 17, Kenga Ramadhan wa umri wa miaka 19 na Juma Kitsao Kazungu wa miaka 18 waliuwawa kwa kupigwa risasi mara kadhaa miilini mwao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Afrika, Khalid Hussein amewataka polisi kukomesha tabia ya kuwapiga risasi kiholela wananchi wasiokuwa na hatia.
Taarifa na Gabriel Mwaganjoni.