Mwakilishi wa Wadi ya Bofu katika eneo la Likoni Ahmed Salama ametiwa nguvuni na maafisa wa kitengo cha kupambana na ulanguzi wa dawa za kulevya Kaunti ya Mombasa akihusishwa na biashara hiyo haramu.
Kamanda mkuu wa polisi wa Kaunti ya Mombasa, Johnstone Ipara, amesema kwamba MCA huyo wa Wadi amehusishwa mno na biashara ya ulanguzi wa dawa za kulevya na maafisa wa kitengo hicho wanaendelea kumhoji sawia na watu wengine 18 waliyotiwa nguvuni katika oparesheni dhidi ya mihadarati iliyozinduliwa mapema jana.
Ipara amesema kwa sasa, wanawazuilia washukiwa hao huku oparesheni hiyo ya saa 24 ya kupambana na ulanguzi wa dawa za kulevya ikipamba moto katika kila pembe ya Kaunti ya Mombasa.
Ipara amewataka walanguzi wa dawa za kulevya kujisalimisha kwa Maafisa wa usalama na dawa hizo vile vile kabla ya nguvu zaidi kutumiwa dhidi yao, akionya kwamba oparesheni hiyo itakuwa kali zaidi.
Katika oparesheni hiyo vile vile watu 7 wametiwa nguvuni katika eneo la Kisauni, watano wakiwa na vifurushi 42 vya dawa za kulevya aina ya heroine huku wawili wakiwa na jumla ya tembe 147 za bugizi.