Takwimu zilizonakiliwa na idara ya afya ya serikali ya Kaunti ya Mombasa kwamba jumla ya watoto elfu 8, 034 walipachikwa uja uzito katika mwaka wa 2018 katika Kaunti hiyo ni za kutisha na kila juhudi zinapaswa kuwekezwa ili kuikabili hali hiyo.
Mkurugenzi mkuu wa Shirika linaloangazia maswala ya vijana la Stretchers Dickson Okong’o amesema kwamba takwimu hizo zinaashiria hali halisi ya ngono za kiholela miongoni mwa Wanafunzi na ukosefu wa habari muhimu zinazofungamana na maswala ya ngono na maradhi ya zinaa miongoni mwao.
Kulingana na Okong’o, Athari za hali hiyo zimeonekana bayana kabisa akihoji kwamba Kaunti ya Mombasa itadidimia kimaadili, kiuchumi na kiuongozi iwapo haitadhibitiwa.
Mwanaharakati huyo wa maswala ya Vijana hata hivyo anasema kwamba Shirika hilo likishirikiana na Serikali ya Kaunti ya Mombasa litazidisha hamasa kwa Vijana ambapo mabalozi wa Vijana watazuru nyanjani kufikisha ujumbe huo wa kudhibiti mimba za utotoni katika Kaunti hiyo.