Story by Ali Chete –
Wanaharakati wa maswala ya kijamii katika kaunti ya Mombasa wameitaka idara ya usalama kukoma kuwatishia na kuwakandamiza watetezi wa haki za kibinadamu katika kaunti hiyo.
Wanaharakati hao wakiongozwa na Mwenyekiti wao Zedekia Adika wamesema idara ya usalama imekuwa ikihujumu harakati zao za kutetea haki za binadamu kutokana na mikakati yao ya kuikosoa idara hiyo kila mara sawa na kukashfu uongozi duni nchini.
Adika amehoji kwamba wanaharakati hao hawatanyamaza hadi pale viongozi watakapo kuwa waadilifu na kuhakikisha kuna kuwa na ugavi sawa wa rasilimali nchini.
Kauli yake imeungwa mkono na Mwenyekiti wa Shirika la First Business Community ambaye amewahimiza wanaharakati hao kutoogopa na kujitokeza kila mara kukashfu uovu unaotekelezwa na serikali.
Kauli za wanaharakati zimejiri baada ya baadhi ya watetezi wa haki za kibinadamu katika kaunti ya Mombasa akiwemo Mwenyekiti wa shirika la MUHURI kuagizwa kufika katika ofisi za idara ya upelelezi na kuandikisha taarifa kwa tuhuma za uchochezi.