Wizara ya utalii na biashara katika serikali ya kaunti ya Kilifi, imewasilisha mswada katika bunge la kaunti hiyo, wakushinikiza kuchukuliwa kwa hatua za kisheria watalii wanaofanya kazi katika kaunti hiyo bila vibali.
Waziri wa Utalii na biashara katika serikali ya kaunti hiyo Nahida Mohamed, amesema baadhi ya watalii wanafanya kazi katika hoteli za kaunti hiyo kinyume cha sheria, akisema kazi hizo zinaweza kufanywa na wenyeji.
Nahida ameongeza kuwa vijana wengi katika kaunti ya Kilifi wamekosa ajira, huku akiwahimiza wawekezaji kutoka mataifa ya kigeni, kutowasahau wenyeji wa maeneo hayo kila wanapotoa nafasi za ajira.
Kwa upande wake Kamishna wa kaunti ya Kilifi Magu Mutindika ameahidi kushirikiana na maafisa wa polisi kufanya msako ili kuwanasa watalii wanaohusishwa na madai hayo.
Taarifa na Marieta Anzanzi.