Wakaazi watakaoathirika na ujenzi wa bwawa la Mwache katika eneo la Kinango kaunti ya Kwale wameitaja fidia ya shilingi elfu 350 kwa kila ekari ya ardhi kama fedha chache kwa wao za kuanza maisha mapya katika maeneo mengine.
Wakiongozwa na Mwakilishi wa Kike wa kaunti ya Kwale Bi Zuleikha Hassan, Waathiriwa hao wameikosoa Serikali kwa kuwapuuza na kutosikiza lalama zao kuhusu swala hilo la fidia.
Kulingana na Zuleikha, licha ya yeye binafsi kuwasilisha lalama hizo bungeni, hakuna mwafaka wowote ambao umepatikana hadi sasa huku wakaazi hao wakiamrishwa kuondoka kabla ya kukamilika kwa mwaka huu.
Wakati uo huo, Kiongozi huyo amemsihi Rais Uhuru Kenyatta kuhakikisha haki na usawa katika swala la fidia kabla ya mradi huo kutekelezwa.
Mradi huo wa maji wa kima cha shilingi bilioni 20 utanarajiwa kuanza kutekelezwa rasmi mwezi machi mwaka wa 2021.