
Msanii Mbosso kutoka Tanzania. Picha/ Kwa hisani
Tunapozifunga pazia za mwaka 2018 ni mengi ningependa kuyasema ila niruhusu nizungumzie jambo moja tu.
Nataka tuzungumze kumhusu Mbosso. Kwa wasiomjua ni msanii kutoka Tanzania chini ya lebo ya Wasafi inayoongozwa na Diamond Platinumz. Kwa nini tumzungumzie Mbosso, wauliza?
Karibu nikupe jibu. Licha ya kuwa msanii mwenye bidii na anayejituma yupo na hulka ambayo itakapoigwa na wasanii wetu italeta natija katika burudani.
Ana hulka gani? Ana hulka ya kuthamini shabiki.
Hivi majuzi akiwa katika Festival ya Wasafi alimtafuta shabiki wake Mzee Jamal maarufu kama “Anacheka Anaona Raha” kutoka Shikaadabu Likoni, Kaunti ya Mombasa.
Yaani lifikirie hili, Mbosso akatoka Tanzania na cha muhimu kwake ilikuwa kumwona Anacheka? Mbosso anatupa somo la kuthamini Shabiki.
Kutokana na kitendo chake hiki mashabiki wamepata sababu ya kumpenda hata zaidi. Hii ni siri iliyo wazi kwetu, wasanii tuthamini mashabiki wetu.
Muwe na mwaka mpya mwema.
Taarifa na Dominick Mwambui.