Mjadala kuhusu wimbo unaowakosoa vikali viongozi wa kisiasa nchini uliyoimbwa na mwanamuziki Kennedy Ombima kwa jina maarufu ‘King Kaka’ na unaofahamika kama ‘Wajinga Nyinyi’ unaendelea kuzua hisia mseto kutoka kwa Wananchi mashinani.
Hisia za hivi punde na kutoka kwa kundi la wasanii wa muziki wa kufoka Mjini Mombasa likiongozwa na Derrick Amunga wanaoshikilia kwamba ‘King Kaka’ ameweka wazi uovu unaotawala nchi na kuwataka Wakenya kubadilisha uongozi huo ili kulinda raslimali ya umma.
Kulingana na msanii huyo, ni sharti wasanii wakome kutumiwa na wanasiasa hasa wakati wa kampeni za uchaguzi na badala yake kuihamasisha vilivyo jamii mashinani ili ifuatilie majukumu ya wanasiasa hao na kuhakikisha wanawahudumia wakenya waliyowapigia kura.
Kwa upande wake, Msanii wa uchoraji John Muthiani amesisitiza umuhimu wa wakenya kutekeleza majukumu yao na kubadili hali ya uongozi nchini badala ya kutumiwa kama vibaraka wa Wanasiasa.
Wimbo wa Msanii Kennedy Ombima unaofahamika kama ‘Wajinga Nyinyi’ umezua mjadala mkali mno huku Wakenya wakimuunga mkono Ombima kwa kuangazia swala la ufisadi bila uoga.