Taarifa na: Gabriel Mwaganjoni
Lamu Kenya, Juni 6 – Ni sharti Wakaazi na Viongozi wa Ukanda wa Pwani kujipanga kisiasa na kujiandaa vilivyo kwa uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022.
Mwakilishi wa kike wa Kaunti ya Lamu Bi Ruweida Obbo amesema kwamba kamwe sio mapema kwa wakaazi wa eneo hili kujipanga kisiasa kama wanavyodai baadhi ya wanasiasa kutoka maeneo mengine ya nchi.
Kiongozi huyo amesema kwamba siasa za wapwani kutumiwa na makundi au vyama vingine vya kisiasa kutoka maeneo ya bara ili kuwapitisha viongozi wengine na wapwani kusalia wakiomba omba nafasi za kuongozi kamwe hazina msingi tena na mkaazi wa ukanda huu anahitaji kujiongoza mwenyewe.
Ruweida amesisitiza kwamba ni lazima swala la uongozi na siasa kujadiliwa vilivyo na wakaazi wa eneo hili kujiweka tayari katika kupigania nafasi zao za uongozi wa nchi bila ya kusubiri kupangiwa na wanasiasa kutoka maeneo mengine ya nchi.