Wakaazi katika ukanda wa Pwani wameshauriwa kuweka mikakati na mbinu za kuhifadhi maji ya mvua kwa matumizi mbalimbali nyakati za ukame.
Akizungumza katika kongamano la 54 la kutathmini hali ya hewa ilivyokuwa mwaka uliopita sawia na utabiri wa miezi mitatu ijayo, afisa katika shirika la ICPAC ,Anthony Musili amehoji kuwa kaunti ndogo ya malindi,kaunti ya Kilifi ilirekodi kiasi kikubwa cha mvua zaidi ya ile iliyotarajiwa.
Musili ameitaka jamii kuwekeza katika uhifadhi wa maji kwani maji mengi ya mvua huwachwa pasi na kuhifadhiwa ilhali yangeweza kutumika katika manufaa mengine nyakati za ukame.
Musili ameongeza kuwa kutokana na utafiti imebainika kuwa Kenya kwa jumla ilipokea mvua kubwa zaidi ya kawaida jambo lililopelekea shinikizo kuhusiana na umuhimu wa kuhifadhi maji.
Musili vilevile ameitaka jamii kuzingatia taarifa za utabiri wa hali ya hewa kwa kile alichokitaja kuwa ni njia mojawapo ya kuepuka na majanga yanayosababishwa na hali ya hewa mbali na kuweka mikakati ya kufanikisha shughuli za kila siku ikizingatiwa kwamba kila mmoja huhitaji habari hizi.