Kumekuwa na kihoja baada ya waombolezaji katika eneo la Bamba kaunti ndogo ya Ganze kuubeba mwili wa ajuza wa miaka 94 na kuuwacha katika kituo cha polisi cha Bamba kwa zaidi ya masaa manne baada ya maafisa wa polisi kuwakataza kucheza disco.
Kulingana na Muthawali Nyuchi jirani ya marehemu Kadzo Ngombo ni kuwa maafisa wa polisi walifika katika Kijiji cha Bamora hapo jana muda mchache tu baada ya maiti kuwasili kutoka chumba cha kuhifadhi maiti na kubeba vyombo vya muziki huku wakidaiwa wakiitisha shilingi alfu sita kabla ya kuwaruhusu kupigisha ngoma hiyo.
Kwa ghadhabu waombolezaji wote waliamua kuubeba mwili huo na kuuacha katika kituo cha polisi cha Bamba huku wakimtaka mkuu wa kituo hicho kuuzika mwili huo.
Akithibitisha kisa hicho mkuu wa polisi wa eneo la Ganze Patrick Ngeywa amesema tukio hilo limechochewa na mmoja wa wanasiasa katika eneo hilo huku akikanusha madai ya maafisa wa polisi kuitisha hongo ili kuruhusu kuchezwa kwa muziki.
Haya yanajiri baada ya Gavana wa kaunti ya Kilifi Amason Kingi na kamishina Magu Mutindika kupiga marufuku upigishaji wa disco kutokana na ongezeko la mimba za mapema kwa wasichana washule na kuzorota kwa kiwango cha elimu.
Taarifa na Marrieta Anzazi