Mwenyekiti wa Chama cha Jubilee kaunti ya Mombasa Matano Chengo amewaonya vikali viongozi wa kisiasa wa kaunti ya Kilifi, akidai kuwa watakabiliwa kisheria endapo watashirikiana na mabwenyenye wa kiwanda cha Saruji cha Athi river kule Kaloleni.
Chengo anasema ni jukumu la viongozi hao kuwa mstari wa mbele kupinga ombi la kiwanda hicho la kutaka kupewa nafasi na Wizara ya Madini nchini ili kupanua shuhuli zake za uchimbaji saruji katika eneo hilo.
Akizungumza na Wanahabari njini Mombasa, Chengo amesema hatua ya viongozi hao ni yakushangaza kwani itawanyima haki na makao wakaazi wa eneo la Maereni kule Rabai.
Chengo amesema endapo kiwanda hicho kitapewa nafasi ya kuendeleza shughuli zake basi ni vyema iwapo wenyeji watapewa nafasi ya mazungumza na kuhamasisha kuhusu athari za shuhuli za kiwanda hicho.
Itakumbukwa kuwa Mnamo tarehe 18 mwezi Julai mwaka huu, Kiwanda hicho kiliwasilisha ombi la kutaka kupewa idhini ya upanuzi wa utendakazi wake kwenye ardhi ya maeneo hayo kikidai kuwa na lengo la kuiboresha sekta ya viwanda hicho.
Ombi hilo limeonekana kupingwa na baadhi ya viongozi akiwemo Kamishna wa Tume ya uiano na utangamano wa kitaifa NCIC, Morris Dzoro aliyeihimiza Wizari ya Madini nchini kutokubali ombi la kiwanda hicho, akitaja kama litahujumu haki ya wenyeji wa maeneo hayo.
Taarifa na Hussein Mdune.