Story by Salim Mwakazi –
Mamlaka ya Mazingira nchini NEMA imewahimiza wakaazi wa kaunti ya Kwale kujitokeza na kupanda miti kwa wingi ili kuafikia asilimia 10 ya idadi ya misitu nchini.
Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo kaunti ya Kwale Godfrey Wafula amesema hatua hiyo itachangia zaidi uboreshaji wa mazingira ya nchi huku akiwataka wakaazi wanaoishi katika maeneo ya Kinango na Lungalunga kuzingatia upanzi wa miti.
Wafula, amesema idadi ya misitu katika maeneo ya Kinango na Lungalunga ingali bado iko chini mno kutokana na uhaba wa mvua na ukataji wa miti kiholela.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa idara ya Mazingira kaunti ya Kwale Joseph Indo amesema kaunti ya Kwale ina kiwango cha asilimia 6.7 ya idadi ya misitu huku akisema tayari wamepanda miti elfu 75 katika mashamba ya wakulima na shule mbali mbali za kaunti ya Kwale.