Story by Our Correspondents-
Mataifa mbalimbali ulimwenguni yameungana na taifa la Kenya kuadhimisha siku ya kimataifa ya utoaji wa damu duniani huku kauli mbui ya mwaka huu ikiwa ni jiunge na juhudi na uokoe maisha.
Shirika la Afya duniani WHO, limeyahimiza mataifa yote ulimwenguni kuunga mkono shinikizo la kuwahimiza wananchi wao kujitokeza na kutoa damu kwa hiari ili kuziwezesha hifadhi za kitaifa za damu kuwa na damu ya kutosha.
WHO, inasema idadi kubwa ya watu duniani wamepoteza maisha yao hospitalini kutokana na ukosefu wa damu katika hifadhi za damu za kitaifa huku ikisema ni wakati sasa kwa mataifa yote duniani kuunga mkono swala hilo.
Nchini Kenya, Wizara ya Afya nchini imejitokeza na kuwasihi wakenya kujitokeza na kuchangisha damu kwa hiari, ikisema tayari zoezi la kuwahamasisha wakenya kuhusu umuhimu wa utoaji wa damu linaendelea ili kuiwezesha hifadhi ya damu ya kitaifa kuwa na damu ya kutosha.
Wizara hiyo imesema juhudi hizo zitachangia hifadhi za damu za kitaifa kuwa na uharaka wa kuwasaidia wagonjwa wanaohitaji damu wakati wa dhararu huku akisema iwapo wadau mbalimbali wataendeleza hamasa kwa jamii basi changamoto hizo zitakabiliwa.