Story by Gabriel Mwaganjoni –
Baadhi ya Wanajeshi wa ulinzi nchini KDF wameripotiwa kuaga dunia huku wengine wakijeruhiwa vibaya baada ya gari lao kukanyaga kilipuzi kilichozikwa ardhini katika eneo la Baure kaunti ya Lamu.
Kamishna wa kaunti ya Lamu Irungu Macharia amethibitisha tukio hilo, akidai kwamba wanajeshi hao wamepoteza maisha yao wakati wakishika doria katika eneo hilo ambalo ni kati ya msitu wa Boni.
Macharia amesema tayari usalama katika eneo hilo umeimarishwa kwani maafisa zaidi wa jeshi la ulinzi nchini KDF wametumwa kushika doria katika eneo hilo huku vilipizi zaidi vilivyozikwa ardhini wanamgambo wa Alshabab vikiteguliwa.
Wakati uo huo jeshi la ulinzi nchini KDF limewataka wakaazi wa eneo hilo kutohofia lolote kwani usalama umeimarishwa huku polisi wakiwasaka wanagambo wa Alshabab wanaozika vilipuzi ardhini.
Tukio hilo limejiri majuma mawili tu baada ya watu wawili kufariki huku mmoja akijeruhiwa vibaya baada ya gari walilokuwa wakisafiri kukanyaga kilipuzi kilichozikwa na Alshabab katika eneo la Border point karibu na kijiji cha Ishakani eneo la Lamu Mashariki.