Story Gabriel Mwaganjoni-
Wakereketwa wa haki za kibinadamu kaunti ya Mombasa chini ya mwavuli wa Okoa Mombasa wameitaka Serikali kuweka wazi stakabadhi zote zinazofungamana na mradi wa SGR.
Wakereketwa hao wamesema licha ya mahakama kuamuru Serikali kutoa stakabadhi hizo serikali bado imedinda kutii amri ya Mahakama.
Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Shirika la MUHURI Khelef Khalifa, wakereketwa hao wamehoji kwamba mradi huo wa SGR umepelekea wakenya kutozwa kodi za juu ili kuugharamia mradi huo.
Katika mkao na wanahabari katika afisi za Shirika hilo eneo la Nyali kaunti ya Mombasa, Khalifa amemkosoa mkuu wa Sheria nchini Paul Kihara kwa kutishia kufika mahakamani ili kuzima juhudi za watetezi hao wa haki za kibinadamu.
Mradi huo wa reli ya kisasa al-maarufu Standard Gauge Railway-SGR uliigharimu Serikali kima cha shilingi bilioni 450, na umetajwa kuwa mradi wa kipekee nchini uliyogahrimu kiasi kikubwa cha pesa katika Serikali ya Jubilee.