Story by Ali Chete& Salim Mwakazi-
Wanaharakati wa kijamii katika ukanda wa Pwani wamewataka wanasiasa kufanya kampeni zao kwa Amani ili taifa hili lishuhudie amani hata wakati wa uchaguzi.
Wakiongozwa na Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Haki Africa, Hussein Khalid, Wanaharakati hao amewataka wanasiasa kukoma kueneza siasa za chuki na ukabila kwani huchangia taifa kushuhudia vurugu.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya amani yalioandaliwa kaunti ya Mombasa, Khalid amesema iwapo viongozi watazingatia hadhi ya taifa hili basi wakenya watashuhudia taifa la amani.
Naye mkurugenzi wa Shirika la Sisters for Justice Naila Abdallah amewataka wakaazi kushikamana na kuishi kwa Amani huku akidokeza kwamba wanaharakati hao wana mikakati ya kuhakikisha jamii inafahamu umuhimu wa utangamano.
Katika kaunti ya Kwale Naibu Kamishna kaunti ya Kwale Alexander Mativo amewaoya wazazi dhidi ya kuwaficha wahalifu na badala yake kuwaripoti kwa maafisa wa usalama akisema hatua hiyo itazidi kuchangia amani nchini.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Amani katika gatuzi dogo la Matuga Mwanakombo Jarumani ameulaumu ukosefu wa ushirikiano baina ya polisi na wananchi akisema hatua hiyo ndio imechangia ukosefu wa amani.