Wanaharakati wa Amani kanda ya Pwani, wamedhihirisha wasiwasi wao kufuatia malumbano makali ya kisiasa katika kampeni za uchaguzi mdogo wa eneo bunge la Msambweni kaunti ya Kwale.
Wakiongozwa na Mkurugenzi mkuu wa Shirika la kijamii la ‘KECOSCE, Bi Phyllis Muema wanaharakati hao wametaka malumbano hayo na cheche za maneno kusitishwa mara moja.
Kulingana na Bi Muema, ni lazima kura ya Msambweni ziwe za uwazi, huru na haki na wakaazi kuwezeshwa kupiga kura kwa amani bila ya kushurutishwa na wanasiasa..
Wakati uo huo, ameutaja uchaguzi huo kama mtihani mkubwa kwa wakaazi wa eneo bunge hilo, akiwataka kubadili mfumo wa uchaguzi wa viongozi nchini unaozingatia misingi ya vyama vya kisiasa.
Uchaguzi huo mdogo wa eneo bunge la Msambweni unaandaliwa juma lijalo siku ya Jumanne tarehe 15 ya mwezi huu wa Disemba.